Ripoti ya Kampuni ya Lugumi kudaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi imerudishwa kwenye kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza sakata hilo baada kubaini mapungufu.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, (PAC) Aeshi Hillaly alisema baada ya kukamilisha ripoti hiyo itapelekwa katika kamati yake ili iweze kujadiliwa.
“Kamati ndogo yenyewe iligundua kuwa kuna mapungufu kwenye hiyo ripoti, kwa hiyo imeirejesha tena kwao ili kurekebisha mapungufu hayo kabla ya kuileta kwenye kamati yangu tuijadili,” alisema.
PAC iliunda kamati hiyo ndogo iliyokuwa inaongozwa na Japhet Hasunga (Vwawa-CCM), ambayo imepewa kazi ya kuchunguza undani wa mkataba huo wenye thamani ya Sh37 bilioni.
Aprili 23, mwaka huu, PAC ilikutana na kuteua wajumbe tisa watakaounda kamati ndogo kuchunguza sakata hilo kwa undani, na kuandaa hadidu za rejea za kufanyia kazi.
Baadhi ya adidu za rejea zilizojadiliwa na PAC ni pamoja na kuangalia thamani ya vifaa vilivyonunuliwa na hali halisi ya soko na kama kulikuwa na ulazima wa kutoa kazi hiyo kwa mbia mmoja.
Kampuni hiyo ilitakiwa kufunga mashine 108 katika vituo vya polisi lakini ilifunga 14 tu.