PROF. Muhongo asherehekea siku ya kuzaliwa kwa namna yake, Haijawahi kutokea hii




Atoa magari matano ya wagonjwa Roli moja
Vitabu 22,000 kwa Shule zote za msingi na Sekondari, Kuwaletea wabunge wenzake bila kujali itikadi ya vyama.
Aahidi madawati 8000, kesho kukabidhi 1,812.
Aleta Madaktari Bingwa kutoka China.

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, leo tarehe 25 Juni 2016 ameadhimisha siku yake ya kuzalisha kwa namna tofauti kabisa huku chakula cha mchana kikiwa ugali na sato.

Prof Muhongo ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, ameiadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kuwakaribisha Madaktari Bingwa kutoka China.
Madaktari hao bingwa watatoa matibabu na dawa bure kwa wanavijiji jimboni humo kwa siku mbili kuanzia leo.
Katika siku hiyo ya kuzalia iliyoadhimishwa kwa aina yake, Prof Muhongo amegawa zaidi ya vitabu 22,000 kutoka Marekani (thamani: US $ 250,000), sawa na TSh500m.
Vitabu hivyo vimesambazwa katika shule za msingi 108 na Sekondari 20.

Lunch ya UGALI NA SATO

Katika sherehe hiyo, Profesa Muhongo aliandaa chakula cha mchana, ambapo yeye na wageni waalikwa walikula ugali na sato katika kijiji cha Kigera.

Waziri Muhongo aliitumia siku hiyo kukabidhi vitu mbalimbali alivyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi wa Rais na Wabunge uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Jimbo la Musoma Vijijini limekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya, elimu, barabara na mabadiliko ya tabia nchi.
Kufuatia mwaliko wa Waziri Muhongo, Madaktari Bingwa Sita kutoka nchini China wako jimboni na tayari wameanza kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi wa jimboni humo.
Madaktari hao wameanza kutoa huduma hiyo katika Zahanati ya Mugango iliyopo kijiji cha Nyangoma, ikiwa ni awamu ya pili kufuatia huduma kama hiyo kutolewa na Madaktari wengine kutoka China mwezi Machi mwaka huu.
Akizindua huduma hiyo ya matibabu Awamu ya Pili, Profesa Muhongo alisema huduma hiyo ni bure na wananchi hao hawatalipia matibabu hayo yanayotolewa leo na kesho.

Profesa Muhongo alisema Madaktari hao wamebobea katika magonjwa ya Wanawake, Watoto, Meno, Vinywa na koo.
Aliongeza kwamba Madaktari wengine ni mabingwa wa macho, kisukari, presha, tumbo na upasuaji wa uvimbe kichwani na tumboni.
“Nimeleta rafiki zangu kutoka China na watawatibu kwa muda wa siku Mbili,” alisema Prof Muhongo.
Aliwaambia wananchi hao kuwa Madaktari hao wanaojitolea walikuja na rafiki zao kutoka China ambao wamewaletea kalamu na vitabu.

“Wamewaletea vitabu vya Sayansi, Hisabati, na Kiswahili, kwa ajili ya kugawa katika shule tano za Msingi, pamoja na mipira itakayogawiwa katika shule hizo na pia kwa timu za mpira za vijiji hivyo,” alisema Mbunge huyo msomi wa jiolojia.



Profesa Muhongo alisema kuwa vitabu hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 500, vimetolewa msaada na marafiki zake kutoka Marekani.

“lengo langu ni kuhakikisha kuwa wananchi katika Jimbo hili mnaelimika na kujenga utamaduni wa kujisomea, hivyo mbali na wanafunzi wetu, hata wananchi mnakaribishwa kuja kuvisoma,”alisema Profesa Muhongo.

Naye Mwakilishi kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, aliyejulikana kwa jina la Bw Zhang, alisema kuwa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi za Tanzania na China ndiyo umewafanya Madaktari hao kuja nchini kutoa huduma za matibabu.
“Ushirikiano wetu unazidi kupanuka na wanachi wengi wa China wanakuja Tanzania kufanya biashara, hali kadhalika wananchi wa Tanzania wanaenda China kwa masuala ya Bishara na Utalii, kwa ushirikiano huu tutazidi kuupanuka katika nyanja za kiuchumi,” alisema Zhang.

Alisema kuwa hadi sasa kuna Madaktari zaidi ya 20 kutoka China wanaotoa huduma za utabibu nchini ambao wapo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tabora, Mara na Dodoma.

“Hii yote inatokana na urafiki na undugu uliopo kati ya nchi hizi mbili, uliojengwa na Mwalimu Nyerere na Mao Tse Ntung,” aliongeza.

Wakati huohuo Profesa Muhongo amezindua ugawaji wa vitabu zaidi ya 22,000 katika Shule za Msingi na Sekondari za Jimbo la Musoma vijijini. Uzinduzi huo umefanywa katika shule ya msingi Kwibara katika kata ya Mugango.
Mbunge huyo alisema kuwa shule zote za msingi 108 na Sekondari 20 jimboni humo zatapata vitabu hivyo.

“Kila shule ya msingi itapata maboksi ya vitabu mawili huku kila shule ya sekondari ikipata maboksi 16,” alifafanua.

ATOA LORI NA MAGARI YA WAGONJWA



Profesa Muhongo alisema kuwa katika kutimiza ahadi zake, amewapelekea wananchi wa jimbo laki gari aina ya Canter.
Gari hilo litatumika kwa ajili ya katika shughuli za misiba, ujenzi wa shule, maabara na vituo Vya Afya.
Tayari Mbunge huyo ameshatimiza ahadi yake ya gari la kubebea wagonjwa ambapo mwezi Machi, 2016 alikabidhi Gari hilo kwa hospitali ya Murangi.
“Leo nawataarifu kuwa baada ya wiki mbili nitawaletea gari nyingine 4 za kubebea wagonjwa na zitagawanywa katika zahanati za Kurugee iliyoko kata ya Bukumi na Zahanati ya Masinono iliyoko kata ya Bugwema.
Gari nyongine za wagonjwa zitapelekwa katika Zahanati ya Mugango katika kata ya Mugango na Zahanati ya Nyakatende katika kata ya Ifulifu.

VITABU VINGINE VINAKUJA

Vilevile alisema kuwa bado kuna vitabu vingine vinavyoendelea kuletwa nchini ambapo awamu nyingine ya tatu inategemewa kufika mwezi Agosti mwaka huu.
Baadhi ya vitabu hivyo atavigawa katika Majimbo mengine ya Mkoa wa Mara bila kubagua itikadi ya Chama kwani wananchi wote wana haki ya kupata maendeleo.
Alisema awamu ya 4 ya vitabu inategemewa kufika nchini mwezi Octoba, 2016.
“Mbunge wetu ameanza na kasi kubwa, ndani ya miezi sita ametimiza ahadi zake na kuzidi, huyu Bwana ni mchapakazi na atatufikisha mbali sana,” alisema Nyambarilo. 
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top