Mchumi: TRA haiwezi Kukusanya Kodi ya Majengo

Mchumi na mtafiti wa uchumi amesema uamuzi wa Serikali kuipa Mamlaka ya Kodi (TRA) kazi ya kukusanya kodi ya majengo badala ya halmashauri za wilaya, utapunguza mapato hayo kutokana na upungufu wa rasilimali watu.


Akitoa maoni yake kuhusu bajeti ya mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni juzi, mchumi huyo, Simon Mapolu alisema TRA haitamudu kukusanya mapato hayo kwa ufanisi kutokana na kuhitaji mtandao mpana wa watumishi kuweza kufanya kazi zilizokuwa zikifanywa na halmashauri za wilaya, manispaa na majiji.


“Halmashauri za wilaya zina watumishi hadi ngazi ya mtaa kwa maana ya wenyeviti na watendaji wa mitaa au vijiji ambao wanatumika kufuatilia na kukusanya ushuru wa majengo, wakati TRA watumishi wao huishia ngazi ya wilaya na maeneo machache kwenye vituo maalumu,” alisema Mapolu.


“Wakati Sheria ya Kodi ya Mwaka 2004 inawafanya TRA kuwasubiria walipakodi wawafuate ofisini, mamlaka za halmashauri huwafuata walipa kodi ya majengo hukohuko waliko.”


Kuhusu ongezeko la kodi kwenye vinywaji baridi na vikali, mchumi huyo alisema ni kasumba inayolemaza wataalamu wa uchumi wa Serikali kufikiria kuongeza kodi kwenye bidhaa hizo kila mwaka badala ya kubuni vyanzo vipya.


“Kwa mfano, kiwango cha kodi kilichoongezwa kwenye vileo na vinywaji baridi kingekusanywa maradufu iwapo nguvu zaidi zingeelekezwa kwenye huduma za simu, kama miamala ya fedha kwa njia ya mtandao,” alisema Mapolu.


Alisema ukiacha miamala ya fedha, makampuni ya simu pia yanaingiza mamilioni ya fedha kupitia gharama za miito ya simu na runinga kwa njia ya mtandao ambayo haijakatwa kodi kwa kiwango kinachostahili.


“Kuna zaidi ya Watanzania 30 milioni wenye kumiliki namba za simu, hawa wakiweka muda wa maongezi ya Sh1, 000 kwa siku, makampuni hayo huingiza zaidi ya Sh3 bilioni kwa siku bila kutozwa kodi stahiki,”alisema Mapolu


Kuhusu Sh50 milioni zilizotengwa kwa kila kijiji kwa ajili ya mikopo kwa wanawake na vijana, mtaalamu huyo alisema ni lengo jema, lakini akaonya kuwa haiwezi kuleta tija iwapo hakutakuwa na mkakati thabiti na unaoeleweka.


Alisema fedha zilizotolewa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na kubatizwa jina la “Mamilioni ya JK”, zilipotea kutokana na kutokuwepo na mfumo wa kuzifuatilia.
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top