Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amesema, ingawa idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na uhakika wa maisha yao wala kazi zenye tija na staha wapo katika nchi zinazoendelea, dunia katika ujumla wake inapashwa kuonyesha utashi wa kisiasa na udhubutu wa kuwekeza kupitia vijana.
Amesema, mazingira ya mamilioni ya vijana kukaa bila shughuli ya aina yote kunatoa mwanya kwa vijana hao kurubuniwa na kutumiwa na watu wasiokuwa na nia njema na hivyo kutishia hali ya Amani, usalama na ustawi wa mwanadamu na hatimaye kushindwa kufikia au kupata faida za kidemografia na maendeleo endelevu.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo ( jumanne) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, wakati alipotoa mhadhara wa 13 wa kumbukumbu ya Rafael M. Salas. Mhadhara huu ambao mada yake ilikuwa ni “ kuwekeza kwa vijana ili kupata faida ya kidemografia na maendeleo endelevu” uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu( UNFPA) ikiwa ni sehemu ya mikutano ya mwaka ya Bodi za Mashirika na Mifuko iliyopo chini ya Umoja wa Mataifa.
Miongoni wa viongozi waliohudhuria na kushiriki mhadhara ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson, na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dr. Babatunde Osotimehin , Bi. Carmelita R. Salas ambaye ni Mjane wa Bw. Rafael Salas aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa UNFPA, Mabalozi na wataalamu mbalimbali.
“Tafiti na taarifa mbalimbali zikiwamo za Umoja wa Mataifa, zinaonyesha wazi ongezeko la idadi kubwa ya vijana wanaokadiriwa kufikia 1.8 bilioni idadi ambayo ni hazina na raslimali kubwa, lakini pamoja na uwingi wao, wengi bado wanaishi katika hali ya umaskini uliokidhiri, na ukosefu wa fursa mbalimbali ambazo zingewazesha kuishi maisha yenye staha”. akasema Kikwete.
Na kuongeza kuwa, kati ya vijana hao 1.8 bilioni, 74 milioni hawana ajira akiwaelezea kama vijana wanaosubiri treni kando ya reli, treni ambayo haiji. Mazingira haya yanadhihirisha upotevu wa raslimali kubwa ambayo imewekezwa kwa vijana hao na ambao wamepoteza matumaini.
Akafafanua zaidi kwa kutoa takwimu mbalimbali zinazoonyesha tofauti ya faidia za kidemografia kati ya mabara ya Ulaya, Asia, Amerika ya Latini na Afrika ikiwa ni pamoja na utofauti wa matumizi ya raslimali watu kwa nchi zile ambazo zimethubutu kuwekeza kwa vijana.
Rais Mstaafu Kikwete katika mhadhara wake huo na ambao ulipokelewa vema sana na wajumbe waliohudhuria, pia ametoa vielelezo vya kitakwimu vinavyoainisha namna gan bara la Afrika lilivyo nyuma karibu katika ikielemewa kila eneo kuanzia upatikanaji na utoaji wa huduma za uzazi salama, idadi ya wakunga wenye elimu ya kutosha, upatikanaji wa huduma za afya, elimu, maendeleo ya kijamii na yenye tija na stahiki na kiwango cha matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.
“Vijana wakiwezeshwa, wakiaminiwa, wakipewa fursa na wakithubutishwa wanauwezo mkubwa sana wa kuleta mabadiliko. Tunatakiwa kuwaamini, tunatakiwa kuwashirikisha na kusizisikia sauti zao” amesema.
Na kuongeza kuwa , mipango na sera zinazoandaliwa kwaajili yao vijana ni vema zikawa shirikishi na kuzingatia mawazo, maoni na matakwa ya vijana.
“Haya na mengi mengi yakitekelezwa kwa kuzingatia mazingira ya kila nchi na vipaumbele vyake, tunaweza kugema nguvu kazi hii kubwa kujiletea maendeleo endelevu pasipo kumwacha yeyote nyuma”akasisitiza Rais Mstaafu.
Katika hotuba yake hiyo iliyosheni takwimu na utafifi wa kisayasi, siyo tu kwamba imeainisha hali halisi ya mazingira waliyomo vijana bali pia imechochea majadiliano na takafuri ya kina.
Baadhi ya mambo ambayo ameyatilia mkazo ni pamoja na umuhimu wa jamiii kuzingatia uzazi salama na wa mpango na kuwa na idadi ndogo ya watoto na ambayo wazazi wataweza kuimudu na elimu itakayokidhi mahitaji ya soko la ajira lishe bora na uchumi imara na endelevu.
Akimkaribisha Rais Mstaafu kuzungumza, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Elliason pamoja na mambo mengine alimwelezea Mhe. Kikwete kuwa ni kiongozi mpenda amani na aliyemstari wa mbele katika kusimamia afya ya mama na mtoto.