Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Akagua Mradi Wa Mabasi Ya Mwendokasi (DART) Jijini Dar Leo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua utendaji kazi kwenye mabasi ya mwendokasi yanayotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam na<endelea bofya kichwa cha habari hii juu> kubaini changamoto kadhaa ambazo amesema zitarekebishwa kadri mradi unavyoendelea.

Waziri Mkuu ambaye alilipa nauli na kupanda basi namba 23 lenye usajili namba T125 DGW kuanzia kituo cha Ferry, Kivukoni, ametumia muda wa dakika 50 kufika Kimara mwisho kwa kutumia usafiri huo.

Waziri Mkuu alipanda basi hilo saa 3:30 asubuhi na lilianza safari saa 3:33 baada ya kusubiri wengine wapande. Kwa wastani ililtumia kati ya dakika mbili hadi tatu kutoka kituo kimoja hadi kingine. Basi hilo liliwasili Kimara Mwisho saa 4:23 asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa Kimara mwisho mara baada ya kumaliza ziara hiyo fupi ya ukaguzi leo (Ijumaa, Mei 27, 2016), Waziri Mkuu alisema aliamua kufanya ziara hiyo ya ghafla ili kuangalia matumizi ya njia za mabasi yakoje na pia kuona abiria wanaelewa vizuri namna ya kuitumia huduma hiyo.

Amesema ameridhishwa na mradi unavyofanya kazi ila ameelezwa kuna usumbufu kwenye mageti wakati abiria wanapotaka kuthibitisha tiketi zao hasa wakati wa asubuhi kunapokuwa na msongamano wa abiria. Pia alielezwa kwamba kuna baadhi ya abiria wanakuja na tiketi za jana yake jambo ambalo linaleta usumbufu kwa sababu hazitambuliki kwenye mfumo wao.

“Nimeridhishwa na uharaka wa njia kwa sababu na mimi mwenyewe nimetumia dakika 50 kufika hapa ingawa kuna maeneo nimeona kuna haja ya kuwa na taa maalum za kuzuia magari (special sensors) wakati mabasi yakipita ili kuepusha ajali,” alisema.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na mtaa wa Samora, Morogoro na Jamhuri na makutano ya Morogoro na Kisutu.

Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waende na tiketi rasmi badala ya kutumia tiketi za jana kwa sababu kufanya hivyo ni makosa na mtu anakuwa amedhamiria. 

“Hawa watachukuliwa hatua za kinidhamu. Mtu akija na tiketi ya jana akamatwe na kupelekwa polisi, huyu atakuwa amedhamiria,” alisema Waziri Mkuu wakati akiongea na mhudumu mmoja katika kituo cha Kimara Mwisho.

“Ninawasihi wananchi wanaotumia usafiri huu wajifunze kufuata utaratibu na kuwasisitizia kuwa kila abiria aje na tiketi ambayo ni rasmi,” alisema na kuongeza: “Haya mabasi nimebaini yako vizuri. Ninatoa msukumo kwa watumishi wa umma wapande mabasi haya ili kupunguza msongamnao wa magari barabarani.”

Katika kupiunguza baadhi ya changamoto, Waziri Mkuu alisema Serikali itasimamia uboreshaji wa ukataji tiketi ili kuondoa usumbufu kwa abiria. Pia alivionya vyombo vya moto viache kutumia njia maalum ya mabasi hayo.

Pia aliwataka polisi wanaofanya doria za usiku kupita kwenye fly-overs na kuwaondoa watu wanaolala kwenye maeneo kwani wanahatarisha usalama wa watu wanaotumia njia hizo. “Zile siyo sehemu za kulala, wanaofanya hivyo wanahatarisha usalama wa watumiaji wa njia hizo, kwa hiyo polisi wakiwakuta watu wa aina hiyo wawakamate mara moja,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga ambaye alifuatana na Waziri Mkuu kaktika ziara hiyo, alisema amepiga marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali.

“Tulishapiga marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali, ninawasihi madereva watambue hili na watii,”alisema.

Machi 22, mwaka huu Waziri Mkuu alitembelea soko la Feri kwa lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo (kuzuia moshi) na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.

Aprili 15, mwaka huu, Waziri Mkuu alifanya kikao na kuwaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pindi majaribio yakianza.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akizungumza na mwanafunzi Amina Abdallah wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Ukombozi jijini Dar es salaam ambaye amepanda basi la Mwendo Kasi Ajentina na kushuka Manzese, Katikati ni Bw. David Mwaibula aliyekuwa Mwenyekiti Mamlaka ya Usafiri wa Daladala Dar es salaam (DRTLA) zamani 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akifurahia jambo wakati Mkurugenzi wa DART Bw. David Mgwasa akisamimiana na Bw. David Mwaibula aliyekuwa Mwenyekiti Mamlaka ya Usafiri wa Daladala Dar es salaam (DRTLA) zamani 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top