Dar es Salaam. Huitaji kuzunguka kwenye mapori ninapolitaja jina la staa, Wema Sepetu kwa<endelea bofya kichwa cha habari hii juu> sababu anafahamika na watu wengi ndani na nje ya nchi.
Mazungumzo kumhusu ni mengi, lakini kwa uchache katika mahojiano aliyofanya na jarida hili, alizungumza mambo mengi ikiwamo kuzindua mfumo wa kupata taarifa zake kupitia Wema Sepetu Mobile App (WSMA), uhusiano wake na Idris, anavyozichukulia dhihaka dhidi yake, anapenda mtoto wa jinsia gani na safari ya maisha yake kwa ujumla.
Mwandishi: Nini lengo la kuanzisha mfumo huu wa kupata taarifa zako?
Wema: Lengo ni kuwapa mashabiki wangu taarifa za ukweli na uhakika zinazonihusu mimi, wakati huohuo nitakuwa naingiza kipato.
Mwandishi: Kati ya drama zako nyingi, ipi iliwahi kukuumiza?
Wema: Ukiachilia mbali yale ya kifamilia, nakumbuka mwaka 2007 nikiwa ndiyo kwanza naanza kuingia katika hii dunia yenye watu wanaojua wenzao kuliko wanavyojijua wao, nikakutana na gazeti lina kichwa cha habari “Wema ana pepo la ngono”.
Kilichonisikitisha ni kwamba (huku anacheka), hata hayo mambo ya mapenzi yalikuwa bado hayajachanganya kiasi cha kuandikwa hivyo.
Nyumbani nilimuacha marehemu baba na mama, nilinunua lile gazeti lakini hata kuwaonyesha nilishindwa.
Da Kalunde (mwandishi wa makala haya) nina moyo wa nyama kama watu wengine, watu wakiniona nje wanajua mimi siumii, wengine wanasema eti nawapa fedha wenye magazeti ya udaku waniandike hilo jambo siyo kweli.
Huwa nalia sana nikiwa ndani ingawa nikitoka nje najikaza na kupotezea, napenda kulia kila linaponifika jambo la kukwaza.
Mwandishi: Unajisikiaje ukiitwa mgumba?
Ni neno linaloniumiza kiukweli na wanaoniita hivyo wamebaini kuwa huo ni udhaifu wangu, nahitaji kupata mtoto tena siyo baadaye sasa, sitaki mtoto wangu achanganye majina kati ya mimi na bibi yake, nataka atofautishe kwa kuona nani bibi nani mama kulingana na umri na mwonekano.
Mwandishi: Uko wapi ukweli wa kuwa na ujauzito na kutokuwa nao?
Wema: Anainamisha kichwa chini kama anayefikiria jambo halafu kwa sauti iliyo poa anajibu: Mimba ilikuwapo kweli ilitoka ikiwa na wiki 13, iliniuma kwa sababu nilitumia dawa za hospitali na mitishamba kwa miaka minne kutafuta japo mimba lakini sikupata. Akiwa na uso wenye huzuni kidogo... Sikuwa nafahamu kama nina ujauzito, nilikuwa nina ahadi na daktari ya kwenda kusafishwa kwa ajili ya kutafuta ujauzito kama ambavyo nimeshasema nimehangaika kuitafuta kwa miaka minne.
Daktari aliponiambia niende siku inayofuata kwa ajili ya kusafishwa nikamueleza kuwa sijapata hedhi kwa muda wa mwezi na siku kadhaa, akaniambia ninunue kifaa cha kupima choo kidogo ili kujiridhisha, niliponunua na kupima niliona mistari miwili ilihali nilizoea kuona mmoja.
Nilishtuka sana na kuwaonyesha rafiki zangu na kama kuwehuka hivi, nikaenda kupima hospitali ili kujiridhisha ni kweli nilikuwa ni mjamzito.
Siku ambayo sipendi kuikumbuka ni ile niliyokwenda msalani na kuona damu ikinitoka, nilipompigia mama yangu alinilaumu badala ya kunipa pole.
“Wema nilikuambia mimba haitangazwi! Unaona sasa kilichotokea , niliyajua madhara ya kufanya hivyo!
Sikuwa na jinsi ikawa ndiyo imetokea kitu cha kwanza nilikaa mbali na mitandao ya kijamii, nikatoka Twitter , Instagram, Whatsapp kwa sababu nilijua wataniua kwa presha.
Mwandishi: Ulizichukuliaje, unazichukuliaje dhihaka za kuhusu ujauzito huo?
Wema: Kwanza sikuwa katika mitandao ya kijamii wakati huo, lakini hata baada ya kurudi siku na haja ya kufuatilia hayo zaidi ya kuangalia afya yangu ikiwamo kupunguza mwili kwa sababu nilinenepa sana.
Mwandishi: Utatangaza jambo hilo tena?
Wema: Siwezi kabisa kufanya hivyo nimekoma, (huku akijiapiza) na hata nikiwa nayo sitapiga picha (ultra sound) kwa ajili ya kutambua jinsi gani ingawa natamani wa kiume awe wa kwanza. Ikifika miezi nane ndiyo nitaanza kufikiria nitampa jina gani. Nikipata wa kike jina ninalolipenda ni Karma.
Mwandishi: Safari za hospitali kwa ajili ya vipimo ulikuwa unaongozana na nani?
Wema: Kichekoo... na Idris. Alikuwa na mimi bega kwa bega kwa sababu alikuwa anaufahamu ukweli na kilichotokea.
Mwandishi: Uko pamoja na Idris kama wapenzi?
Wema: Yap! Tupo pamoja ila tunapendana sana ndiyo maana tunagombana mara nyingi, lakini tupo pamoja na itabaki kuwa hivyo.
Mwandishi: Uliwahi kuandika waraka mrefu ukimlenga Zari (Mpenzi wa Diamond)
Wema: Ukiona nimefikia hapo ujue nimechoshwa na maneno maneno. Ni kweli nilifanya vile ili kufunga mjadala. Sina matatizo naye na ninamuombea heri katika penzi lake.
Mwandishi: Katika maisha yako ya kila siku huwa haifiki wakati unamkumbuka Diamond?
Wema: Kumkumbuka kimapenzi hapana! kumbuka kuna Nassib na Diamond. Mimi nilikuwa kwenye mapenzi na Nassib na tumeshamalizana sasa hivi nimebaki kuwa shabiki wa Diamond ambaye kusema ukweli anafanya vizuri na mimi kama Mtanzania ninajivunia kuwa anatuwakilisha vyema nje ya mipaka ya nchi yetu.
Mwandishi: Kuna kitu kinakukera mwilini mwako hadi unakichukia?
Wema: (Kicheko)...Kipo na ninajutia sana mchoro wa shingoni, ulikuwa mchoro wangu wa kwanza na mchoraji alitumia sindano badala ya wino.
Alichora mchoro kwenye karatasi kama mjusi hivi kwa sababu nilikuwa nina hamu ya kujichora, nikamwambia achore tu kwa sasa siupendi tena. Nilichomwambia nataka mchoro unaoshuka kutoka shingoni kuelekea begani na ndicho alichofanya.
Huu!... una michoro mingapi mwilini hadi sasa?
Wema: Nina michoro saba na ninataka ifike 10, kati ya hiyo mitatu iliyobaki miwili itakuwa ya jina la mwanaume aliyenipa ujauzito na la mtoto wangu wa kiume, mmoja uliobaki sijui nichore nini kutimiza idadi. Kiukweli sijawahi kumchora mwanaume katika mwili wangu nataka kufanya hivyo kwa atakayenipa mtoto kumuenzi tofauti na hapo no...no...!
Mwandishi: Umewahi kuongeza makalio au sehemu nyingine ya mwili?
Wema: Hapana sijawahi kufanya hivyo ninavyoonekana ndivyo nilivyo, nafahamu yanasemwa mengi lakini sijawahi kufanya hivyo. Inawezekana yanasemwa kutokana na ninavyopenda urembo.
Mwandishi: Kati ya viatu, nywele unapenda nini?
Wema: Napenda sana nywele, linapokuja suala la urembo nywele ni kitu cha kwanza kwangu. Nikitaka kujiridhisha na kupendeza nitakavyo mimi huweka nywele hadi ya Sh1.2 milioni na kima cha chini kabisa cha nywele ni Sh150,000.
Mh...anasita na kumtizama Martin Kadinda meneja wake kama anataka amkumbushe kitu halafu anajibu “Napenda kuvaa viatu virefu vinanipa uhuru wa kutembea kwa hatua ninazopenda na kujiamini zaidi, nina viatu jozi zaidi ya 100.
Mwandishi: Huwa unachukua muda gani kujiremba na unakuwa huru ukivaa nguo gani?
Wema: Kama nina mtoko wa kawaida nachukua dakika 10 hadi 20 lakini nikiwa nakwenda kwenye tukio maalumu lazima aje mpambaji na kila kitu usoni huchukua kama saa mbili au zaidi kumaliza. Ili nifurahie vazi nililovaa liwe refu tena gauni, hapo hujiona nipo huru na hujikubali kwa sababu ni la staha na linanipendeza nakuwa kwenye mwonekano mzuri wa kike na kunionyesha uhalisia wa shepu yangu.
Kiukweli nikitoka napenda niwe miongoni mwa waliovaa vyema katika tukio husika angalau niwe namba tatu kati ya waliopendeza katika tukio hilo.
Hivyo ndivyo nilivyo katika mavazi na urembo na acha niseme itabaki kuwa hivyo kama siwezi kuvaa vizuri kwa sababu moja ama nyingine bora nibaki nyumbani kuliko kujikera na kuwakera waliozoea kuniona nimetoka poa.
Swali: Unatumia kilevi gani?
Wema: Natumia mvinyo mara nyingi, lakini linapokuja suala la bia nakunywa Safari kwangu hiyo ndiyo bia hizi nyingine nitakunywa kama maji.
Swali: Ulifanya filamu na wasanii wa nje kama Van Vicker na Omotola zimeishia wapi?
Wema: Filamu ya Super Star ina utata kidogo kwa sababu watu niliofanya nao kazi wameing’ang’ania kwa lengo la kunikomoa ikiwamo kuhitaji fedha niwalipe nyingi kitu ambacho hakiwezekani.
Kuhusu filamu yangu na Van Vicker ipo karibuni kutoka hapo awali ilikuwa itoke Septemba na nikatafuta wadhamini kwa ajili ya uzinduzi lakini Vicker akawa na ratiba ngumu mwaka uliopita na hakutaka mtu mwingine ahariri.
Hivyo niliporudi kwa wadhamini wakati huu wameniambia hadi waone kitu hivyo Vicker amenitumia demo ya dakika 20 ya promo na matayarisho yameanza Inshallah baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani itaingia sokoni.
Swali: Mtu akikuhitaji kwa ajili ya kuigiza filamu yake ajipange vipi?
Wema: Kwanza awe na filamu yenye ujumbe maridhawa na isiwe na magumashi, lakini awe na kitita cha Sh10 milioni hadi 15 milioni , lakini kwa kuwaangalia usoni na ukaribu kuna ambazo ninaweza kufanya hadi Sh7 milioni.
Swali: Unaipenda filamu gani kati ya ulizoigiza?
Wema: Naipenda Lady Valentine na DJ Ben.
Swali: Unaitumiaje mitandao ya kijamii?
Wema: Naitumia vyema ikiwamo kufanya promo ya biashara, unaweza kuamini kama rangi za mdomo za Kiss nimeziuzia mtandaoni kwa asilimia 90? Wengi wetu bado hatuitumii vizuri na ukishiriki sana inaumiza lakini kikazi naitumia.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)